Askari wa usalama barabarani wapongezwa

0
2512

Rais John Magufuli amewapongeza askari wa usalama barabara kwa juhudi zao za kusimamia usalama wa barabarani licha ya changamoto m mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo Septemba 23 alipokutana na kunywa chai na baadhi ya askari hao Ikulu jijini Dar es salaam, muda mfupi baada ya kutoka katika ibada ya jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Nawapongeza Trafiki wote kwa kazi mnazofanya, nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi, mnafanya kazi zenu kwenye jua na mvua, na wakati mwingine mnakwazwa na watumia barabara lakini mnaendelea na kazi.“Nataka kuwatia moyo, chapeni kazi, wanaovunja sheria za barabarani wachukulieni hatua, msitishwe na mtu yeyote lakini na nyie msimuonee mtu yeyote” amesisitiza Rais Magufuli.

Askari hao wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaalika Ikulu kupata nao chai ya asubuhi na kuzungumza nao na wamemhakikishia kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuhakikisha usalama barabarani unazidi kuimarika chini ya kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

“Tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa upendo wako kwetu, umetutia moyo sana na tunakuhakikishia tutachapa kazi kwa nguvu zetu zote” amesema Mkuu wa Trafiki wa Wilaya ya Kipolisi ya Kati Inspekta Neema Mvungi.

Mapema asubuhi, Rais Magufuli ameshiriki misa takatifu iliyoongozwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Oysterbay Padre Bathlomeo Bachoo ambaye katika maombezi yake amewaongoza Waumini kuwaombea Marehemu wote wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere walale mahali pema peponi na majeruhi wapone haraka.