Ashikiliwa kwa mauaji Singida

0
2373

Jeshi la polisi mkoani Singida linamshikilia Naligwa John mwenye umri wa miaka 23 mkazi wa kijiji cha Mgundu wilayani Iramba kwa tuhuma za kumdhalilisha na kumkaba shingo hadi kufa mtoto mwenye umri wa miaka 12 mwanafunzi wa darasa la Nne katika shule ya msingi Mgundu.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, – Sweetbert Njewike amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya mauaji hayo mbele ya mdogo wa marehemu mwenye umri wa miaka Tisa wakiwa wanachunga mifugo.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Singida, Kamanda Njewike amesema kuwa baada taarifa za tukio hilo kumfikia mama mzazi wa marehemu, mama huyo alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi ambao walijitokeza na kuanza kumtafuta mtuhumiwa huyo na hatimaye kumkamata akiwa katika harakati za kutoroka.

Kufutia tukio hilo, Kamanda huyo wa polisi wa mkoa wa Singida ametoa angalizo kwa wazazi wa jamii ya wafugaji kuhakikisha usalama wa watoto wao wanapokua kwenye kazi ya kuchunga mifugo.

Jeshi la polisi mkoani Singida linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.