Rais John Magufuli amewashukuru Viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kumuomba Mwenyezi Mungu ili aliepushe Taifa na janga la corona.
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo hii leo alipokaribishwa kuwasalimu Waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino mkoani Dodoma baada ya kushiriki Misa Takatifu ya Sikukuu ya Utatu Mtakatifu.
Amesema Mwenyezi Mungu amejibu maombi ya Watanzania ambao wamesali, wamefanya toba na kufunga, na matokeo yake ni kuwa maambukizi ya virusi vya corona yamepungua na wananchi wanaendelea na maisha yao huku wakichapa kazi za uzalishaji mali, tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ugonjwa huo ungesababisha madhara makubwa.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa makini dhidi ya mbinu zozote zinazoweza kufanywa kuwaambukiza ugonjwa huo ama magonjwa mengine, huku wakimshukuru na kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote.
Akiwa Kanisani hapo, Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa hilo na kufanikiwa kuchangisha zaidi ya shilingi milioni 17 ikiwemo shilingi Milioni 10 aliyochangia yeye mwenyewe na mifuko 76 ya saruji.
Rais Magufuli ametaka upanuzi wa Kanisa hilo Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino uanze kesho.