Anyongwa na mpenziwe kisa wivu

0
163

Mwili wa Petronel Mwanisawa (22) ambaye alikuwa Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Iringa aliyefariki dunia kwa madai ya kunyongwa na mpenzi wake, unaagwa hii leo chuoni hapo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa, – Juma Bwire amesema kuwa mara baada ya mwili huo kuagwa, utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Bwire amesema kuwa, kwa sasa Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Prudence Patrick (21) Mwanafunzi wa chuo kikuu hicho cha Iringa anayedaiwa kuhusika na mauaji hayo, ambaye amekamatwa katika kituo kikuu cha mabasi cha Iringa akiwa anatoroka baada ya mauaji hayo kuelekea nyumbani kwao Bukoba mkoani Kagera.

Amesema chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni wivu wa mapenzi, ambapo Prudence alikuwa akimtuhumu Petronel kuwa na uhusiano na Mwanaume mwingine ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambaye pia anadaiwa kumpa ujauzito.

Kamanda Bwire amesema mara baada ya kufanya mauaji hayo, Prudence anadaiwa kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa Mama wa Marehemu na kumtaarifu kuhusu tukio hilo.