Mpigania uhuru wa nchini Kenya amekubali kunyoa nywele zake zenye urefu wa mita mbili na kusema matakwa yake kama mpigania uhuru yametimizwa na serikali.
Nywele ndefu ni moja ya alama ya wapigania uhuru ambapo wengi walizinyoa mara tu baada ya kurudi kutoka msituni kama ishara ya kuwepo kwa uhuru, lakini mwanamama Muthoni wa Kirima hakufanya hivyo.
Kirima (92) alikuwa mwanamgambo wa Mau Mau cheo cha ‘Field Marshal’ na rafiki wa Mama Ngina Kenyatta, mke wa Rais wa kwanza wa Kenya na mama wa Rais Uhuru Kenyatta.
Mama Ngina ambaye alimnyoa nywele hizo Kirima amesema amejivunia kunyoa nywele za Kirima na kisha kuzizungushia kwenye bendera ya Kenya na kusema nywele hizo zitahifadhiwa kwenye jumba la makumbusho.