Anayedaiwa kuwa jambazi sugu mbaroni

0
78

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Omary Mchomme (39) dereva wa pikipiki anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu, ambaye anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Mchomme anadaiwa kushirikiana na wenzake kufanya vitendo mbalimbali vya uhalifu ikiwa ni pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Muliro Jumanne amesema, wamemkamata mtu huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa alikua akijiandaa kwenda kufanya uhalifu.

Amesema walianza kumfuatilia na kumkamata katikati ya Kisarawe na Kwembe wilaya ya Ubungo akiwa anajiandaa kwenda kuungana na wenzake ili wafanye uhalifu na alipobaini kuzingirwa na polisi alitoa bastola na kuanza kuwashambulia polisi hao.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, Polisi walijihami na kumpiga risasi moja iliyomjeruhi mguuni na hatimaye kumkamata.

Jeshi la Polisi limebaini kuwa mwaka 2017 mtuhumiwa huyo aliwahi kukamatwa na kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo alihukumiwa miaka 30 jela, lakini mwaka 2019 alikata rufaa na kuachiwa huru.