Anayedaiwa kumuua mkewe na kutoroka akamatwa

0
169

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limemkamata
Isaya Mzava mwenye umri wa miaka 59 mkazi wa Bunju Beach mkoani Dar es Salaam kwa tuhuma za kumuua kwa kutumia kitu chenye ncha kali mke wake Irene Mzava mwenye umri wa miaka 56, mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Muliro Jumanne amedai kuwa baada ya kufanya mauaji hayo terehe 26 mwezi Desemba mwaka 2021, Mzava alitoroka na kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa kutumia gari namba T 727 DKK aina ya Toyota Harrier ambapo alipobaini anafuatiliwa alilitelekeza gari hilo Moshi Mjini na kulekea mkoa wa Arusha.

Amesema Polisi waliendelea kumfuatilia ambapo alikimbilia wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga, na baadaye alikimbia na kuelekea wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambapo alikamatwa tarehe nne mwezi huu katika kijiji cha Kagoma na kurudishwa Dar es Salaam.

Kamanda Muliro amesema Mzava atafikishwa mahakamani haraka iwezekenavyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.