Dereva Teksi Mousa Twaleb mwenye umri wa miaka 46 na Mkazi wa Tegeta jijini Dar es salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, akikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kumteka Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji.
Twaleb amefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Wankyo Simon, amedai kuwa katika shitaka la kwanza, mshitakiwa huyo alijihusisha na genge la uhalifu.
Kadushi amedai kuwa Mei Mosi na Oktoba 10 mwaka 2018 katika maeneo ya jiji la Dar es salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwa makusudi Twaleb alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa kwa lengo la kujipatia faida.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Kesi hiyo
imeahirishwa hadi hadi Juni 11 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa
amerudishwa rumande.
Mohammed Dewji maarufu kama MO alitekwa Oktoba 11 mwaka 2018 majira ya alfajiri
katika maeneo ya hoteli ya Colloseum jijini Dar es salaam wakati akienda kufanya mazoezi
na alipatikana Oktoba 20 mwaka huohuo wa 2018 katika eneo la Gymkhana.
Katika habari
nyingine, ukiwa umepita muda wa mwezi mmoja tangu Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi
yaendayo Haraka katika jiji la Dar es salaam (UDART), – Robert Kisena na wenzake kufikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, upande wa utetezi umeutaka upande wa mashtaka
kukamilisha upelelezi wa kesi inayowakabili ili hatua nyingine ziweze
kuendelea.
Wakili wa utetezi Zuri’el Kazungu ameeleza hayo mahakamani hapo, mbele
ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,- Augustine Rwizire wakati shauri hilo
lilipowasilishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa Serikali Wankyo Saimon amedai kuwa, upelelezi bado unaendelea na kwa
mazingira ya shauri hilo maeneo yanayofanyiwa upelelezi ni mengi hivyo hawawezi
kueleza hatua waliyofikia.
Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Juni Sita mwaka huu na washitakiwa
wamerudishwa rumande.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mke wa Kisena, Frolencia Membe, Kulwa
Kisena, Charles Newe na raia wa China, -Cheni Shi .
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 19 likiwemo la kuisababishia
UDART hasara ya Shilingi Bilioni 2.41.
