Aliyeua Mwanafunzi ahukumiwa kifo

0
517

Mahakama Kuu Kanda ya BUKOBA imemtia hatiani na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa Mwalimu wa shule ya Msingi KIBETA iliyopo mkoani Kagera, –  Respicius Mutazangira  kwa tuhuma za kumuua kwa kukusudia mwanafunzi wa shule ya Msingi Kibeta,  Spelius Eradius Agosti 27 Mwaka 2018.

Akitumia muda wa saa mbili kusoma hukumu hiyo Jaji Mfawidhi Lameck Mlacha amesema mahakama imemuachia huru mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Mwalimu Herieth Gerald baada ya kutokuwepo na ushahidi wa moja kwa moja kumuunganisha na kifo cha Mwanafunzi huyo.

Jaji Mlacha amesema mshtakiwa huyo alitumia fimbo ngumu Tatu  maarufu kama Kuni   kumuadhibu mwanafunzi huyo ambaye alidaiwa kuiba mkoba wa mshtakiwa wa pili Mwalimu Herieth Gerald huku akitoa maneno ya kumtisha kwa muda wa saa Tatu katika eneo la shule na nje ya eneo hilo.

Amesema ushahidi  usio na shaka  wa madaktari  pamoja na mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi umeonyesha kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikuwa na majeraha yaliyotokea muda mfupi na kwamba Mwanafunzi huyo alipewa adhabu ya kipigo kutoka kwa Mwalimu huyo.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa Mwalimu aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa  Respicius Mutazangira ambaye pia alikuwa Mwalimu wa nidhamu katika shule ya Msingi Kibeta alionekana kuishiwa nguvu akiwa kizimbani huku furaha ikijitokeza kwa ndugu na jamaa wa mshtakiwa wa pili Mwalimu Hereth Gerald.