Watu sita wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari aina ya toyota Noah lililogongana na lori aina ya scania katika eneo la Alkatani wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo katika barabara ya Arusha – Babati na kusema kuwa wakati inatokea gari hilo aina ya Noah lilikuwa likitoka Arusha mjini kwenda Karatu na lori lilikuwa linatoka Makuyuni kuelekea Arusha mjini.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alishindwa kulimudu na kuhamia upande mwingine wa barabara ambapo aliligonga gari hilo aina ya toyota Noah.
Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, Jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia dereva wa roli aliyesababisha ajali hiyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kufuatia ajali hiyo, Kamanda Masejo amewaomba Wakazi wa mkoa wa Arusha kufika katika hosptali ya rufaa ya mkoa huo Mount Meru ili kutambua miili ya watu waliofariki dunia.
Pia ametoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto mkoani Arusha kuwa waangalifu wawapo barabarani, lengo likiwa ni kuepuka ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi.