Afrika yatakiwa kuwekeza kwa vijana na watoto

0
452

Mkutano wa siku Mbili wa Africa Now Summit 2019 unaofanyika jijini Kampala nchini Uganda, unamalizika hii leo.

Akihutubia mkutano huo katika siku ya kwanza ya ufunguzi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kuibadili Afrika Viongozi wake lazima wawekeze kwa Vijana pamoja na Watoto.

“Viongozi lazima wahakikishe wanawekeza kwenye lishe bora ya watoto wanaozaliwa na kuhakikisha mifumo yetu ya elimu inalenga katika kutoa elimu bora na yenye kukuza vipaji ili kwenda sawa na ulimwengu wa teknolojia”, amesema Makamu wa Rais.

Aidha amesisitiza Afrika lazima iwekeze kwenye mipango itakayoleta maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo na si mipango kwa ajili ya chaguzi zijazo.

Mkutano huo uliofunguliwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, unalengo la kuwakutanisha Viongozi wa Afrika kujadili masuala mbalimbali ya utengamano katika kuleta maendeleo endelevu Barani Afrika.

Viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Naibu Rais wa Kenya,- William Ruto na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Misri,-Amr Nassar.