Afrika watakiwa kufungua shule zikiendelea kupambana na COVID-19

0
287

Shirika la Afya Dunia pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) yamezitaka serikali za nchi za Afrika kufungua shule na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama wakati wakiendelea kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Taasisi hizo za kimataifa zimebainisha kuwa kuendelea kufunga shule kwa muda mrefu kunapelekea watoto kukumbana na changamoto mbalimbali kama vile mimba za utotoni, ukatili pamoja na kutopata chakula sahihi.

Kiongozi wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti amesema wakati jitihada za kupambana na corona zikiendelea ni vyema nchi zisisahau elimu na kuishia kuwa na kizazi kibaya. Ameongeza kuwa, kama ambavyo biashara zinafunguliwa na kufanyika kwa usalama, basi iwe hivyo kwa shule.

Baadhi ya nchi za Afrika zimeendelea kufunga shule ukiwa ni mkakati wa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo, huku nyingine zikienda mbali kufuta mwaka wa masomo kama ilivyo kwa Kenya, na kuelekeza kuwa wanafunzi wataanza upya mwaka 2021.

Wakati taasisi hizo zikitaka shule kufunguliwa, Tanzania tayari imefungua shule zote kuanzia Juni mwaka huu baada ya maambukizi ya virusi vya corona kupungua kwa kiasi kikubwa.