Afrika Kusini yaihakikishia Tanzania ushirikiano

0
210

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa matukio ya mashambulizi dhidi ya wageni nchini humo sio msimamo wa Serikali ya nchi hiyo na kwamba Serikali hiyo itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa kidugu na kihistoria na Tanzania.

Rais Ramaphosa amemtuma Mjumbe Maalum, -Jeffrey Radebe ambaye ni Waziri wa Nchi Mstaafu wa Afrika Kusini aliyeongozana na Mshauri wa Rais wa Afrika Kusini katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa Dkt Khulu Mbhatha, kuwasilisha barua yenye ujumbe huo kwa Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es salaam.

Katika ujumbe huo, Rais Ramaphosa amefafanua kuwa, Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi na kupigania uhuru ambapo Tanzania ilijitolea kambi na misaada mbalimbali kwa Wapigania uhuru.

Katika mazungumzo na Wajumbe hao, Rais Magufuli amesema kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini na amesisitiza ushirikiano zaidi katika maeneo ya Biashara na Uwekezaji.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amekutana na Mjumbe maalum wa Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Hirut Zemene Kassa.

Mjumbe huyo wa Waziri Mkuu wa Ethiopia,- Abiy Ahmed amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Ethiopia itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema kuwa, Tanzania itadumisha na kukuza zaidi uhusiano wake na Ethiopia katika maeneo mbalimbali ikiwemo ushirikiano katika usafiri wa anga.