Afisa habari atakayezembea kuchukuliwa hatua  

0
180

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amewaagiza maofisa habari, mawasiliano na uhusiano Serikalini kujituma katika kutekeleza majukumu yao, na kuonya kuwa atayezembea hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo jijini Mbeya wakati akifungua kikao kazi cha maofisa habari, mawasiliano na uhusiano wa Serikali, na kutaka kikao hicho  kiwe chachu ya kuboresha utendaji pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika kusimamia utoaji wa huduma za habari kwa umma, ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 na sheria ya haki ya kupata habari ya mwaka 2016.

 Aidha Waziri Bashungwa ametumia kikao hicho kumuagiza Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili maofisa hao ikiwemo kutoshirikishwa kwenye ziara za kutembelea miradi mbalimbali inayotokelezwa na wizara au taasisi zinatatuliwa mara moja. 

Changamoto nyingine ni baadhi ya maofisa habari kuwekwa chini ya kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambapo majukumu yake hayapewi kipaumbele pamoja na kutokuwa na bajeti, vifaa na bajeti ya inteneti na simu.