AfDB kufadhili miradi zaidi Tanzania

0
135

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Adesina Akinumwi amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa benki hiyo itaendelea kufadhili miradi ya maendeleo hapa nchini, na ipo tayari kufadhili miradi mipya.

Dkt. Adesina aliyepo jijini Abidjan nchini Ivory Coast amesema hayo leo wakati akizungumza kwa njia simu na Rais Samia Suluhu Hassan aliyepo Jijini Dar es salaam, ambapo viongozi hao wamejadili uhusiano wa Tanzania na benki hiyo ambayo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ameahidi kuwa AfDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili kuanzisha benki za Wajasiriamali zitakazowakopesha vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kujihusisha na kilimo, jambo litakalosaidia kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato.

Aidha, Dkt. Adesina amemualika Rais Samia Suluhu Hassan  kuhudhuria mkutano wa uwekezaji utakaowakutanisha Wawekezaji wakubwa.

Pia Dkt. Adesina amesema AfDB imetenga dola bilioni tano za Kimarekani kwa ajili ya kusaidia Wanawake, na ameomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshaji Wanawake kiuchumi,  ombi lililokubaliwa na  Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika mazungumzo hayo Dkt. Adesina ametoa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kutoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti cha Urais, na kuongeza kuwa ana matumaini ataendeleza jitihada zilizokuwa zikifanywa na mtangulizi wake.

Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amemshukuru Dkt. Adesina kwa salamu zake za pole na pongezi,  na amemshukuru kwa benki hiyo kufadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa awamu ya pili na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo.

Ameelezea kufurahishwa na mradi wa AfDB wa kufadhili vijana wanaojihusisha na kilimo na wanaomaliza mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi kwa kuwa ufadhili huo utawawezesha vijana wengi wa Tanzania kuzalisha mali.

Pamoja na kumpongeza Dkt. Adesina kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa AfDB kwa kipindi cha pili, Rais Samia Suluhu Hassan amemuomba kuongeza nafasi za Watanzania wanaoajiriwa katika benki hiyo.