Ada yafutwa, wanafunzi vyuo vya kati kupewa mikopo

0
336

Serikali ikiwa imetumia shilingi Bilioni 661.9 kwa ajili ya elimu bila ada pamoja na shilingi Trilioni 1.4 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu hadi Aprili 2023, imeleta ahueni zaidi kwa wanafunzi wa vyuo vya kati pamoja na vyuo vya ufundi ikiwa ni lengo la kukuza wataalamu zaidi.

Akiwasilisha mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba ameliambia bunge kuwa Serikali inakusudia kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi.

Dkt. Mwigulu amevitaja vyuo vitakavyonufaika kuwa ni Dar es Salaam Institute of
Technology (DIT), Mbeya University of Science and Technology (MUST) na Arusha Technical College (ATC), na kwamba hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda (4th Industrial Revolution).

Kama hiyo haitoshi, Waziri Mwigulu amesema Serikali inapendekeza kuanzisha programu ya mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa na Serikali kusoma kwenye vyuo vinavyotoa elimu katika fani za kipaumbele ambazo ni sayansi, afya, ufundi na ualimu.

Hatua hiyo itaanza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2023/24.

Mageuzi hayo yamekuja ikiwa ni miezi michache tangu Serikali ilipoamua kuongeza kiwango cha posho ya kujikimu maarufu kama Boom kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka shilingi 8,500 hadi shilingi
10,000 kwa siku.