Mafunzo ya stadi za kazi kuwanufaisha vijana

0
243

Zaidi ya Vijana Elfu 46 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya Uanagenzi, yanayotolewa  kupitia Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania katika mwaka wa fedha wa 2019/2020.
 
Hayo yamebainishwa hii leo jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akizindua awamu ya Pili ya mafunzo hayo, uzinduzi uliofanyika pamoja na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO).

“Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeandaa Programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kuanzia wahitimu wa darasa la saba hadi vyuo vikuu”, amesema Waziri Mkuu.
 
Mafunzo hayo yanayotolewa kwa njia hiyo ya Uanagenzi, tayari yamefanyika mwaka 2017 na 2018 kwa awamu ya kwanza, ambapo vijana zaidi ya Elfu 32 wamehitimu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, katika awamu ya Pili ya mafunzo hayo iliyozinduliwa hii leo jumla ya vijana 5, 875 watashiriki.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu,-Jenista Mhagama amesema kuwa, hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, jumla ya vijana 36,726 walikua wamefaidika na programu ya kukuza ujuzi inayogharamiwa na Serikali kwa asilimia Mia Moja.
 
Amefafanua kuwa, kati ya vijana hao 6,455 walinufaika na mafunzo ya Uanagenzi katika fani mbalimbali zikiwemo zile za ushonaji wa nguo, useremara, uashi, uchongaji wa vipuri na ufundi magari.