5G Kuwekwa Kwenye Mwendokasi

0
173

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Habari Nape Nnauye amesema maeneo yote ya wazi nchini yatawekewa intaneti ya bure ‘Free Wi-Fi”.

Waziri Nape ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa Baharini wa Airtel-2Africa na huduma ya Intaneti ya 5G.

“Mikoani popote penye Machinga Complex tutaweka Wi-Fi ya bure na kwa Dar es Salaam tutaweka Wi-Fi ya bure kwenye Mwendokasi, sehemu zote ambazo Mwendokasi wa Dar es Salaam unakwenda tutaweka kwa sababu tunataka watu watumie huduma hii.” amesema Waziri Nape.

Ametaja sifa za Mkongo huo wa 2Africa kuwa ni pamoja na kuwa
ndio Mkongo mrefu na mkubwa kuliko yote duniani ambao una urefu wa Kilomita elfu 45 na unaunganisha zaidi ya nchi 30 duniani.

Pia unaunganisha Mabara matatu ambayo ni Afrika, Asia na Ulaya
na unategemewa kuunganisha zaidi ya watu Bilioni tatu Duniani.

“Mikongo yote tuliyonayo ina wastani wa kasi ya 16 TB kwa sekunde, mkongo huu uliozinduliwa una kasi ya 180 TB kwa sekunde mara 11.25 zaidi ya kile tulichonacho.” amesema Waziri Nape na kuongeza kuwa

“Mkongo huu utaongeza kasi ya intaneti nchini zaidi ya mara 10 ya sasa, utasaidia kushusha gharama za mawasiliano nchini. Ni fursa kubwa ya kuvutia kampuni kubwa duniani kama Google, Netflix n.k.”

Wakati wa uzinduzi huo imeelezwa kuwa pamoja na kukuza uchumi wa nchi, Mkongo huo utasaidia kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.