Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema katika kipindi cha mwezi Januari mwaka 2022 hadi Januari mwaka huu watuhumiwa 241 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali kwa makosa ya ulawiti na ubakaji.
Kamanda Masejo ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu
kufikishwa mahakamani kwa mkazi mmoja wa Sombetini jijini Arusha kwa tuhuma za kumdhalilisha mtoto wake mwenye umri wa miaka saba ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza.
Mkazi huyo amekamatwa na kufikishwa mahakamani kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa hivi karibuni baada ya kusambaa kwa taarifa ya mtoto huyo kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na baba yake.
Aidha Kamanda Masejo ametolea mfano tukio la hivi karibuni ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu Kelvin Wilfred (19) mkazi wa Muriet Arusha kifungo cha maisha kwa kosa la kumdhalilisha mwanafunzi mwenye umri wa miaka nane wa darasa la nne.
Amesema jeshi la polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na vyombo vingine litaendelea kuwafuatilia wale wote watakaobainika kutenda matukio ya uhalifu ikiwemo ya ukatili na unyanyasaji katika jamii.