Zimbabwe kuwa na mafuta na gesi asilia

0
2217

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametangaza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta na gesi asilia kaskazini mwa nchi hiyo.

Amesema kuwa kampuni ya uchimbaji madini ya Invictus Energy ya nchini Australia kwa kushirikiana na serikali ya Zimbabwe inatarajiwa kuanza utafiti ili kubaini iwapo mafuta hayo yanaweza kuchimbwa na kuuzwa kibiashara.

Rais Mnangagwa amesema kuwa kisima cha mafuta kitachimbwa na kampuni hiyo ya Invictus Energy kwenye wilaya ya Muzarabani katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

“Tumeshauriwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Invictus Energy kwamba matokeo ya utafiti huo yana matumaini makubwa na yanaashiria kupatikana kwa mafuta na gesi asilia katika eneo hilo” amesema Rais Mnangagwa.

Kisima hicho cha mafuta kitachimbwa takribani kilomita 240 kaskazini mwa mji mkuu wa Zimbabwe, – Harare kwa gharama ya dola milioni 20 za kimarekani.