Takribani watu Thelathini wanahofiwa kufa, baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo katika
mgodi mmoja wa dhahabu nchini Chad.
Waziri wa Ulinzi wa Chad, -Mahamat Abali Salah amesema kuwa, maporokoko hayo ya udongo yametokea kwenye machimbo ya dhahabu ya Kouri Bougoudi yaliyopo katika jimbo la Tibesti.
Habari kutoka nchini Chad zinaeleza kuwa, shughuli za uokoaji zimechukua muda mrefu kutokana na eneo hilo la machimbo kuwa gumu kufikika.
Sababu nyingine inayofanya kazi ya kuwaokoa watu hao wanaodhaniwa kufukiwa na kifusi kufuatia maporomoko hayo ya udongo kwenye jimbo hilo la Tibesti kuwa ngumu, ni kutokana na jimbo hilo kuwekwa katika hali ya tahadhari, kufuatia mashambulio mbalimbali ambayo yamekua yakifanywa na Wanamgambo.
Habari zaidi kutoka nchini Chad zinasema kuwa, eneo ambako maporomoko hayo ya udongo yametokea, limekithiri kwa kuwa na Wachimbaji wengi wa migodi wasiokua na leseni.
