Wapinga kuahirishwa kwa Bunge

0
239

Wanasiasa na Raia mbalimbali nchini Uingereza wameendelea kumshutumu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Borris Johnson, kwa kuahirisha Bunge la nchi hiyo hadi katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu na kusema kuwa kitendo hicho ni ukiukaji wa katiba ya nchi hiyo.

Uamuzi huo wa Waziri Mkuu Johnson, pia umesababisha hasira miongoni mwa Wanasiasa hao na Raia wa Uingereza ambao wameandamana katika miji mbalimbali nchini Uingereza kupinga jambo hilo.

Maandamano hayo yalianzia nje ya ukumbi wa Bunge la Uingereza na kuendelea katika maeneo mengine, ambapo waandamanaji hao wamesema kuwa watafanya maandamano makubwa zaidi mwishoni mwa Juma.

Waandamanaji hao wamedai kuwa hatua ya Waziri Mkuu Johnson ni sawa na mapinduzi dhidi ya serikali ya Uingereza.

Nao Wabunge nchini Uingereza wamesema kuwa, kwa vile nchi hiyo itajitoa rasmi kwenye umoja wa nchi za Ulaya Oktoba 31 mwaka huu, muda uliowekwa na Waziri Mkuu hautoshi.

Hata hivyo baadhi ya wachunguzi wa siasa za Ulaya wamesema kuwa Johnson  ameweka muda huo ili kuzuia mijadala itakayozuia nchi hiyo kujitoa rasmi kwenye Umoja wa Ulaya.