Wanasheria wanawake washinikiza uchunguzi wa polisi waliobaka

0
319

Chama cha Wanawake Wanasheria Malawi kimefungua kesi dhidi ya jeshi la polisi nchini humo kwa kushindwa kuchunguza kesi za ubakaji zilizoripotiwa dhidi ya baadhi ya maafisa wa polisi.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2019 nchini humo kulikuwa na maandamano ya mara kwa mara ambapo wafuasi wa upinzani walikuwa wakipinga mchakato wa uchaguzi, huku wakitaka kuitishwa kwa uchaguzi mpya.

Baadhi ya polisi walitumia upenyo uliotokea kipindi cha maandamamo hasa mwezi wa Octoba 2019 kufanya vitendo vya ubakaji kwa wanafunzi na wanawake katika maeneno ya Msundwe, M’bwatalika na Mpingu.

Kesi hizi ziliripotiwa kwa mamlaka husika na shirika la haki za binadamu liitwalo NGO Gender Coordination Network (NGO-GCN) huko Malawi, huku wakimtaka Rais Peter Mutharika kuingilia kati suala hili kwa kusema hakuna mtu aliye juu ya sheria, lakini jitahada hizo hazikuzaa matunda.

Suala la kufumbiwa macho kwa vitendo hivyo limepelekea Chama cha Wanawake Wanasheria Malawi kujihusisha huku wakiwa na lengo la kuwatendea haki wanawake hao kwa kufungua madai dhidi ya polisi nchini humo.