Zaidi ya wanafunzi 300 waliotekwa nyara na kundi la kighaidi la Boko Haram katika shule ya sekondari ya Kankara Kaskazini magharibi mwa Nigeria wamewasili leo katika jimbo la Katsina.
Gavana wa jimbo la Katsina Aminu Bello Masari amesema wanafunzi hao wa kiume wamewasili katika makao makuu ya jimbo hilo kusubiri taratibu za kupokelewa na familia zao baada ya uchunguzi wa afya zao.
Taarifa zinasema mafanikio ya kurejeshwa kwa wavulana hao yamepatikana saa chache baada ya watekaji kusambaza mkanda wa video unaowaonyesha makundi ya wanafunzi hao waliotekwa nyara wiki iliyopita.
Msemaji wa Gavana wa Katsina amesema video hiyo iliyosambazwa na Boko Haram katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni ya kweli, lakini sauti ya mzungumzaji anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo, Abubakar Shekau ni bandia.
Aidha Labaran amesema hakuna mwanafunzi yoyote aliyeuawa katika tukio hilo la utekaji, kauli inayokinzana na ya mwanafunzi mmoja aliyezungumza katika mkanda wa video wa Boko Haram, akidai kuwa baadhi ya wanafunzi wenzake wameuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege za kivita za jeshi la Nigeria.
Mwaka 2014 kundi hilo la kigaidi la Boko Harama liliwateka nyara pia wanafunzi wa kike zaidi ya 276 huko Chibok, Nigeria na mpaka sasa zaidi wasichana 100 bado hawajarudi nyumbani.