Waliopinduliwa wazuiwa kusafiri

0
283

Jeshi nchini Guinea ambalo limetwaa madaraka baada ya kuipindua Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais Alpha Conde, imewazuia waliokuwa maafisa wa Serikali iliyopinduliwa kusafiri kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Jeshi limechukua hatua hiyo huku Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS),  wakilaani mapinduzi hayo ya kijeshi.

Awali kiongozi wa mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Guinea, Mamady Doubouya aliamuru Mawaziri wote pamoja na Viongozi waliokuwa wakishika nyadhifa mbalimbali kwenda katika ukumbi wa bunge la nchi hiyo mjini Conakry, ili wakashtakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka na mali ya umma.

Alpha Conde mwenye umri wa miaka 83 pamoja na Mawziri na Maafisa kadhaa wa Serikali iliyopinduliwa wanashikiliwa kizuizini.

Wananchi wameonekana mitaani wakiendelea kushangilia na kuunga mkono mapinduzi hayo ya kijeshi, huku hatma ya hali za viongozi waliopinduliwa katika nchi hiyo ya Guinea ikiwa haiijulikani.