Waliokufa katika maandamano Iraq watambuliwa kama Mashujaa

0
956

Serikali ya Iraq imetangaza kuwa, watu wote waliokufa wakati wa maandamano ya kupinga Serikali ya nchi hiyo zaidi ya wiki moja iliyopita kuwa ni Mashujaa, waliokufa wakitetea haki za Wananchi wa Taifa hilo.

Spika wa Bunge la Iraq, -Mohammed Al Halbousi amesema kuwa, Serikali ya nchi hiyo itafanya uchunguzi kuhusu vifo vya Waandamanaji, wengi wao wakiwa ni wahitimu wa vyuo Vikuu waliouawa na Polisi wa kutuliza ghasia.

Watu hao waliokufa baada ya askari wa kutuliza ghasia kutawanya maandamano yao kwa risasi za moto.

Spika Halbousi amesema kuwa, watu wote watakaobainika kuwa waliuawa na askari hao wa kutuliza ghasia, familia zao zitalipwa fidia na Serikali imewatambua rasmi kuwa ni watu waliokuwa wakitetea haki.

Habari zinasema hali ya utulivu imerejea nchini Iraq, baada ya siku kadhaa za maandamano, ambayo mara kadhaa yalisambaratishwa na polisi kwa risasi za moto na kusababisha vifo vya zaidi ya watu Mia Moja.

Maandamano hayo yalianzia mjini Baghdad na kuenea katika miji mingine ya nchi hiyo, ambapo Wahitimu hao wa vyuo Vikuu walikuwa wakiishinikiza Serikali ya Iraq kuwapatia ajira, kwa kuwa kwa miaka mingi wamehitimu vyuo, lakini wanashindwa kuitumia elimu waliyopata.

Spika Halbousi amesema kuwa, madai ya Wanafunzi hao ni ya kweli na walitakiwa kusikilizwa na tatizo lao kutafutiwa ufumbuzi badala ya kutumia nguvu kutawanya maandamano yao, hali iliyosababisha maafa yasiyokuwa ya lazima.