Wakuu wa nchi zaidi ya 10 kuhudhuria mazishi ya Moi

0
349

Zaidi ya Wakuu wa nchi Kumi kutoka sehemu mbalimbali Duniani, wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Kitaifa ya Rais wa PIli wa Kenya Mzee Daniel Arap Moi.

Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Kenya imeeleza kuwa Wakuu hao wa nchi wamekwishathitisha kushiriki katika mazishi hayo ya Kitaifa na kwamba wataanza kuwasili Kenya Jumatatu Februari 10.

Mazishi hayo ya Kitaifa yatafanyika katika uwanja wa michezo wa Nyayo uliopo jijini Nairobi, ambapo tayari Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo amekagua maandalizi yanayoendelea na kueleza kuridhika nayo.

Siku ya Jumanne mwili wa Mzee Moi utapelekwa katika uwanja huo wa Nyayo ukitokea katika jengo la Bunge la nchi hiyo baada ya kulazwa kwa muda wa siku Tatu ambapo umeagwa na maelfu Wananchi wa Taifa hilo

Mara baada ya mazishi hayo ya Kitaifa, mwili wa Mzee Moi utapelekwa nyumbani kwake Kabarak kwa ajili ya shughuli za mazishi rasmi yatakayofanyika siku ya Jumatano.

Miongoni mwa watu waliotoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mzee Moi katika jengo hilo la Bunge ni Rais Mstaafu wa Kenya, – Mwai Kibaki.

Kibaki alihudumu kama Makamu wa Rais kwa muda wa miaka Kumi katika utawala wa Moi na pia kushika wadhifa wa Uwaziri katika wizara mbalimbali.

Mzee Moi aliyeingia madarakani mwaka 1978 alikabidhi kiti cha Urais kwa Kibaki mwaka 2002.