Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kufanyia kazi nyumbani

0
613

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amewaagiza wafanyakazi wote wa makao makuu ya umoja huo kufanyia kazi nyumbani kwa muda wa mwezi mmoja ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Amesema kuanzia machi 16 hadi Aprili 12 mwaka huu, wafanyakazi wote wa makao makuu ya umoja huo huko New York nchini Marekani watafanyia kazi zao nyumbani isipokuwa tu kwa watakaopata dharura itakayowalazimu kufika ofisini.

Guterres ametoa agizo hilo baada ya mwanadiplomasia wa Ufilipino anayefanyakazi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuthibitika kuambukizwa virusi vya corona.

Mwanadiplomasia huyo alikuwa ameshiriki moja ya vikao vya Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa kuanzia machi 16 hadi mwisho wa mwezi Aprili mwaka huu, vikao vingi vilivyokuwa vifanyike kwenye makao makuu ya umoja huo navyo vimesitishwa.

Kampuni mbalimbali na mashirika mengi likiwemo lile la Fedha Duniani (IMF) yamerudisha wafanyakazi wao nyumbani, lengo likiwa ni kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.