Kwa mara nyingine tena waandamanaji nchini Sudan wamepambana na polisi wa kutuliza ghasia, katika maandamano yao ya kupinga serikali, wakiwa wameingia katika siku yao ya nane ya maandamano hayo.
Rais Omar Abashir wa Sudan amewaita waandamanaji hao kuwa wasaliti na kuwataka kuachana na maandamano hayo mara moja. Jana polisi walitumia risasi za moto kuwazuia waandamanaji waliokuwa wakielekea katika ikulu ya nchi hiyo.
Awali waandamanaji waliokuwa wakiandamana kupinga serikali ya Sudan, walikuwa wakiandamana kupinga ongezeko la bei ya mikate na bidhaa za mafuta ya magari, lakini maandamano ya safari hii yamekuwa na sura nyingine.
Waandamanaji wanasema wataendelea na maandamano yao hadi serikali ya rais Bashir itakapoachia madaraka, na kupatikana kwa uongozi mpya. Maandamano mengine yanatarajiwa kufanyika leo nchini Sudan.
Maandamano ya safari hii yamekuwa na sura nyingine, kwani licha ya waandamanaji kushuhudia wenzao wakipigwa risasi na kufa, wamekuwa wakisonga mbele ya kuendelea na maandamano yao.