Raia wa Uganda ambaye pia ni mwanafunzi anayesoma nchini China amekwama kukamilisha safari yake ya kurudi nyumbani baada ya vyombo vya usafiri mjini Wuhan kufungwa ili kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Juliet Nsiima amekiandikia kituo cha habari cha New Vision cha nchini Uganda kwamba alipaswa kuanza safari yake ya kurudi Uganda leo Jumatano, Januari 29 lakini hajafanikiwa kutokana na kukosa usafiri wa kumfikisha uwanja wa ndege.
“Kwa hivyo, ndege yangu ya Guangzhou bado ilikuwa imepangwa kwenda Entebbe. Niliondoka chuo kwenda mjini ili nione hali ya vizuizi ilivyokuwa. Ilikuwa ngumu.
“Mfumo wa usafiri wa umma ulikuwa umefungwa. Hakukuwa na mabasi au teksi kubeba abiria.” ameandika Nsiima.
Kutokana na maambukizi ya virusi hivyo kuzidi kuongezeka nchini China, Nsiima amewaomba wasomaji wa ujumbe huo aliouweka New Vision wamuombee yeye na mamia ya raia wa Uganda waliomo nchini humo ili wawe salama.