Viongozi wa juu wa kijeshi wafukuzwa kazi

0
418


Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amemfukuza kazi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa nchi hiyo pamoja na Mkuu wa Jeshi la anga.

Rais Nyusi amewafukuza kazi viongozi hao wa juu wa kijeshi katika kipindi hiki ambacho vikosi vya nchi hiyo vinapambana na Wanamgambo ambao wanaendeleza mapigano katika eneo la kaskazini la nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Msumbiji haijaweka wazi sababu za kufukuzwa kazi kwa Ezequiel Isac Muianga Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Messias André Niposso ambaye ni Mkuu wa jeshi la anga.

Rais Nyusi pia amewafukuza kazi Kamanda na Naibu Kamanda wa chuo cha Kijeshi cha Marechal Samora Machel na kuwabadilisha kazi maafisa wengine wa ngazi ya juu katika vyuo mbalimbali vya kijeshi.

Tangu mwaka 2017, vikosi vya Msumbiji vimekuwa vikikabiliana na na vikundi vya Wanamgambo  katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini la Cabo Delgado na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.