Viongozi mbalimbali watuma salamu za pole

0
397

Salamu za pole zimeendelea kutolewa kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na raia wote wa nchi hiyo,  kufuatia kifo cha Rais wa Pili wa Taifa hilo Mzee Daniel arap Moi kilichotokea  hii leo.

Salamu za hivi karibuni zimetoka kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Jane Marriott,  Balozi wa Marekani nchini Kenya, Kyle McCarter, na kiongozi  wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.

Viongozi hao wote wamemuelezea Mzee Moi kuwa katika kipindi chake cha uongozi aliheshimu misingi ya demokrasia na kusimamia haki za binadamu.

Katika salamu zake za pole kwa Taifa la Kenya, Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema Mzee Moi kuwa alikua kiongozi wa mfano kwa vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.

Naye Rais Dkt. John Magufuli kwa niaba ya Watanzania wote  tayari ametuma salamu za pole  kwa Rais Uhuru Kenyatta raia wote wa nchi hiyo kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu.

Rais Magufuli amesema kuwa, Tanzania itamkumbuka Mzee Moi kwa uongozi wake mahiri, jitihada zake za kuimarisha uhusiano wa kidiplomaisa baina ya mataifa hayo mawili, pamoja na jitihada zake za kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).