Viongozi mbalimbali wameendelea kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliokufa baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kuanguka na kuwaka moto.
Salamu za hivi karibuni zimetoka kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza,- Thereza May na Waziri Mkuu wa Canada ,-James Trudeau ambao kwa pamoja wameeleza kusikitishwa na ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwamo ndani ya ndege hiyo.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737-MAX 8, imeanguka katika mji Bishoftu nchini Ethiopia, dakika sita tu baada ya kuruka ikiwa katika safari zake za kawaida kutoka Addis Ababa Ethiopia kuelekea Nairobi nchini Kenya ikiwa na abiria 149 na Wafanyakazi Wanane.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Ndege la Ethiopia inasema kuwa idadi kubwa ya abiria waliokufa inadhaniwa walikuwa wanakwenda jijini Nairobi kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa unaohusu mazingifa unaotarajiwa kuanza hii leo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, abiria waliokufa katika ajali hiyo ya ndege, 32 ni raia wa Kenya, 18 wanatoka Canada, Tisa wa Ethiopia , China Nane, Italia Nane, Marekani raia Nane , Uingereza Saba, Ufaransa Saba na Misri Sita.
Wengine ni kutoka Uholanzi Watano, Russia watatu, Morocco wawili, Israeli wawili na mmoja mmoja kutoka nchi za Ubelgiji ,Uganda, Yemen, Sudan, Togo , Msumbiji na Norway.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) David Beasley amesema kuwa Wafanyakazi Saba wa shirika hilo ni miongoni mwa watu walikufa kwenye ajali hiyo.
Kufuatia ajali hiyo ya kuanguka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, Serikali ya nchi hiyo imetangaza siku ya leo kuwa ni ya maombolezo ili kuwakumbuka watu wote waliokufa.