Muungano wa majimbo 16 nchini Marekani ukiongozwa na jimbo la California umeushtaki mahakamani utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuhusu uamuzi wake wa kutangaza hali ya dharura ili kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta ambao ni mpaka wa nchi hiyo na Mexico.
Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama moja iliyopo katika jimbo la California na imefunguliwa zikiwa zimepita siku kadhaa baada ya Trump kuidhinisha hali ya dharura inayompa nguvu ya kulivuka bunge na kupata fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
Mkuu wa sheria katika jimbo hilo la California, – Xavier Becerra amesema kuwa wameushitaki utawala wa Rais Trump mahakamani kwa kuwa kutangaza hali hiyo ya dharura ni matumizi mabaya ya nguvu za Rais.
Trump alitangaza hali hiyo ya dharura ili kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta ambao ni mpaka wa Marekani na Mexico baada ya bunge la nchi hiyo kukataa kuidhinisha ujenzi huo.
Akitoa tangazo hilo, Trump alisema kuwa hatua hiyo itamuwezesha kupata takribani Dola Bilioni Nane kwa ajili ya ujenzi huo.