Uongozi mpya nchini Sudan

0
177

Baraza Huru litakaloiongoza Sudan kurejea katika utawala wa kiraia linaanza kazi hii leo, baada ya sherehe za kuapishwa kwa Wajumbe wa Baraza hilo.

Hatua hiyo inafuatia kuundwa rasmi kwa baraza hilo linalojumuisha Wajumbe Watano kutoka Jeshi la Sudan na wengine Sita kutoka muungano wa makundi ya upinzani.

Habari kutoka nchini Sudan zinasema kuwa, Baraza hilo Huru litaiongoza Sudani katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu, ambapo Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ataliongoza kwa siku za awali.

Luteni Jenerali Burhan ndiye aliyeiongoza Sudan baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa madarakani Rais Omar Al-Bashir mwezi Aprili mwaka huu.

Waziri Mkuu wa Sudan, naye anatarajiwa kuapishwa hii leo.

Pande hizo Mbili zilitia saini makubaliano ya kuunda serikali ya mseto mwishoni mwa wiki iliyopita, makubaliano yaliyojumuisha uundwaji wa Baraza Huru na namna ya kupokezana uongozi ndani ya Baraza hilo.

Mwishoni mwa muda wa uongozi wao, Wajumbe hao wa Baraza huru la Uongozi nchini Sudan wanatarajiwa kuandaa uchaguzi huru utakaorejesha utawala wa kiraia.