Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu imewaonya viongozi wa nchi mbalimbali duniani kutokiuka haki za binadamu kwa kutumia nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.
Katika taarifa yake, ofisi hiyo imewataka viongozi hao kutambua kuwa tishio kubwa ni virusi vya corona na si watu.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa (UN) inayoshughulikia Haki za Binadamu imetoa taarifa hiyo huku kukiwa na habari kuwa vikosi vya baadhi ya nchi zikiwamo Afrika Kusini, Kenya, Uganda na Rwanda vimekua vikitumia nguvu kubwa ili kuhakikisha wananchi wanachukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema vitendo ambavyo vimekua vikifanywa na vikosi vya usalama vya kuwapiga risasi, kuwakamata raia na kuwaweka vizuizini kwa madai kuwa wanakiuka taratibu wakati wa mapambano dhidi ya corona havikubaliki.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 32,000 barani Afrika wameugua homa ya mapafu (COVID-19) ambapo 1,428 kati yao wamefariki dunia.