Umoja wa Mataifa waipongeza Tanzania

0
1201

Umoja wa Mataifa umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mchango wake wa kulinda amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, na kuahidi kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo katika masuala mbalimbali.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, – Antonio Guterres alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York nchini Marekani.

Wakati wa mazungumzo yao, Guterres na Waziri Kabudi wamegusia masuala ya maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa nchini Burundi na hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa unatambua mchango na jitihada za Tanzania na kuongeza kuwa Umoja huo upo tayari kushirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kuzuia matukio mbalimbali hasa yale ya uhalifu.

Kwa upande wake Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi ameuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja huo  katika vikosi vya kulinda amani vilivyopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na sehemu nyingine duniani ili kuufanya Ukanda wa Maziwa Makuu, Afrika na Duniani kwa ujumla kuwa mahali salama pa kuishi.

Ameongeza kuwa Tanzania inaunga mkono mabadiliko yanayofanyika ndani ya Umoja wa Mataifa.

Profesa Kabudi ametumia mazungumzo yake na Guterres kumueleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya Tanzania ili kujiletea maendeleo pamoja na watu wake.