Ulinzi waimarishwa Indonesia

0
506

Ulinzi umeendelea kuimarishwa nchini Indonesia, baada ya watu Sita kuuawa wakati wa maandamano yaliyokuwa yakiambatana na ghasia ya kupinga matokeo ya uchaguzi Mkuu yaliyompatia ushindi Rais Joko Widodo wa nchi hiyo.

Waandamanaji wanaoongozwa na mpinzani mkubwa wa Widodo,- Jenerali Prabowo Subiento wanadai kuwa,  kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wakati wa kupiga kura,  hivyo matokeo hayo si halali na wataendelea na maandamano.

Subiento amekuwa akiwahamasisha wafuasi wake kuendelea na maandamano ambayo yamekuwa yakiambatana na ghasia,  hali iliyosababisha polisi wa kutuliza ghasia kutumia nguvu kutawanya maandamano hayo.

Widodo amewaonya waandamanaji hao kuwa serikali yake haitakubali kuona uvunjifu wa amani ukiendelea nchini humo na yuko tayari kufanya kazi na watu wanaotaka kulijenga taifa hilo.

Amesema kuwa taratibu za kupinga matokeo nchini humo ziko wazi, ambapo walalamikaji wanapaswa kwenda mahakamani kulalamika na sio kutumia ghasia kama sababu za kupinga matokeo.

Serikali ya Indonesia imesema kuwa inafanya uchunguzi kuhusiana na watu waliokufa wakati wa maandamano hayo, kwani askari wake walikuwa wakitumia risasi za mpira kutawanya waandamanaji pamoja na mabomu ya kutoa machozi.

Hata hivyo wataalamu wa masuala ya silaha wamesema kuwa mabomu hayo yakipigwa kwa umbali mfupi pia yanaweza kusababisha madhara yakiwemo vifo.