Papa Francis ametahadharisha kuwa dunia inafikia hatua ya kupuuzia majanga na maumivu kiasi kwamba yanatokea na hakuna hatua zinazochukuliwa kuyadhibiti.
Katika ujumbe wake wa Krismasi amegusia migogoro inayoendelea Syria, Yemen na Iraq pamoja na maeneo mengine ya Afrika, Ulaya na Asia.
Ameeleza kuwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19) limezorotesha jitihada za kimataifa za utatuzi wa migogoro hiyo ambayo inasababisha maumivu kwa watu wengi.
Ametumia jukwaa hilo pia kutahadharisha juu ya athari za kijamii za UVIKO19 na kueleza kwamba tabia ya watu kutokukutana na kufanya mambo pamoja inakuwa kwa kasi, hivyo huenda ikaathiri ustawi wa jamii na ushirikiano.
“Katika ngazi ya kimataifa kuna hatari pia ya kuepuka mazungumzo, jambo ambalo janga hili litasababisha watu kuchukua njia za mkato badala ya kuchukua njia zenye manufaa ya muda mrefu kutatua matatizo,” amesisitiza Papa.
Amehutubia maelfu ya waumini wa Kikristo waliokusanyika eneo la wazi la St Peter’s Square mjini Vatcan.