Uganda: Waziri adaiwa kupiga watu risasi baada ya kushindwa kura za maoni

0
384

Waziri wa Ajira nchini Uganda, Mwesigwa Rukutana anatarajiwa kufikishwa mahamani leo baada ya kukamatwa mwishoni mwa wiki kwa tuhuma za kuwafyatulia risasi wafuasi wa mpinzan wake.

Waziri huyo anatuhumiwa kuwapiga risasi wafuasi wa mpinzani wake baada ya kushindwa katika kura za maoni kupitia chama tawala, National Resistance Movement (NRM).

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa watu watatu wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Licha ya mashuhuda wa tukio hilo kusema kuwa kiongozi huyo aliwafyatulia risasi wafuasi hao baada ya kuchukua bunduki ya msaidizi wake, Rukutana amekanusha kutenda kosa hilo.

Kaimu Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, Polly Namaye amesema mtuhumiwa huyo pamoja na walinzi wake watatu watashtakiwa kwa kosa la jaribio la kuua.

Uganda inajiandaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka 2021.