Tetemeko jingine la ardhi lenye ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter limetikisa aneo la Kusini la Uturuki, zikiwa zimepita siku kadhaa tangu kutokea kwa tetemeko jingine katika nchi hiyo pamoja na Syria na kusababisha vifo vya watu takribani elfu 46.
Taasisi inayoshughulikia maafa nchini Uturuki imeeleza kuwa tetemeko hilo limetokea majira ya jioni hii leo kwa saa za Afrika Mashariki.
Watu walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa tetemeko hilo limesababisha uharibifu hasa wa majengo katika mji wa Antakya.
Wataalamu wa masuala ya miamba wamesema baada ya kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi tarehe 6 mwezi huu lenye ukubwa wa 7.8, Uturuki imekumbwa na matetemeko mengine madogo zaidi ya elfu sita, lakini la leo limekuwa ni kubwa zaidi.
Tetemeko hilo la leo pia limeitikisa miji kadhaa katika nchi za Syria, Misri na Lebanon.
Mpaka sasa hakuna taarifa zaidi kuhusu madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo.