Tanzania na UNAIDS kuendeleza ushirikiano

0
174

Serikali ya Tanzania imefikia makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti Ukimwi (UNAIDS) kuendelea kushirkiana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha pembezoni cha 75 cha Shirika la Afya Duniani kati ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na Mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima.

Waziri Ummy ameeleza kuwa Tanzania inajivunia ushirikiano imara, wa kimkakati na wenye manufaa na msaada kutoka kwa UNAIDS katika nyanja za uongozi, uundaji wa sera, na ukusanyaji wa rasilimali kwa ajili ya mwitikio wa kitaifa wa mapambano dhidi ya VIrusi vya UKIMWI.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Byanyima ameupongeza utawala bora chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, na kuahidi kuendelea kushirkiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Aidha, Byanyima amemshukuru Rais Samia kwa kukubali kuwa kinara wa uhamasishaji wa uchangiaji wa mzunguko wa saba wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).