Tanzania Makamu Mwenyekiti mpya wa SADC

0
2821

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umemalizika rasmi tarehe 18 Agosti katika mji wa Windhoek nchini Namibia kwa kumteua Rais John Magufuli kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 mpaka Agosti 2019.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyemwakilisha Rais Magufuli katika mkutano huo ameishukuru SADC kwa imani kubwa waliyoionesha kwa Tanzania katika jukumu hilo na amewaahidi Wakuu nchi wanachama ushirikiano wa dhati wa serikali ya Tanzania katika kutekeleza majukumu ya Makamu Mwenyekiti kwa kuweka mbele vipaumbele na agenda za Jumuiya hiyo.

Kufuatia uteuzi huo, Rais Magufuli atapewa rasmi jukumu la Uenyekiti wa SADC katika Mkutano Mkuu ujao wa 39 utakaofanyika Tanzania mwezi Agosti mwaka 2019.

Tanzania imeteuliwa kushika nafasi hiyo kufuatia utaratibu wa kawaida wa mzunguko wa uongozi baina ya nchi Wanachama wa SADC ambapo itaongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2018 hadi Agosti 2019.

Viongozi wengine walioteuliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Jamhuri ya Namibia kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 hadi Agosti 2019.

Troika ya SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 na Agosti 2019 itaundwa na Namibia, Tanzania na Afrika Kusini.