Sudan Kusini yachunguza chanzo cha ajali za ndege

0
174

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameagiza kusimamishwa kwa shughuli zote zinazofanywa na Shirika la ndege la South Supreme la nchini humo, ikiwa ni siku moja tu baada ya ndege yake moja kuanguka na kuua watu wote kumi waliokuwamo ndani.

Katika taarifa yake Rais Kiir amesema shughuli za kampuni hiyo zinasimamishwa kwa muda katika kipindi hiki unapofanyika uchunguzi, kubaini chanzo cha kuanguka mara kwa mara ndege zinazomilikiwa na mashirika mbalimbali ya ndege ya nchini humo.

Amesema uchunguzi huo ni muhimu kwa kuwa utatoa majibu ya hali halisi ya usafiri wa anga katika maeneo mbalimbali nchini Sudan Kusini, ambao kwa sasa umekuwa ukitiliwa shaka.

Ndege hiyo iliyokuwa katika safari zake za kawaida kutoka jimbo la Jonglei kuelekea mji mkuu wa Sudan Kusini, – Juba, ilianguka katika uwanja wa ndege wa Pieri mara tu baada ya kuruka.

Wakati ajali hiyo inatokea, ndege hiyo ndogo ya abiria ilikuwa na watu 10 ndani ambao ni abiria pamoja na marubani wawili.