Watu sita wamekufa na wengine hamsini wamejeruhiwa baada ya kukanyagana kufuatia kuzuka kwa taharuki katika tamasha la muziki wa kufokafoka kwenye klabu moja ya usiku nchini Italia.
Maafisa wa uokoaji na zimamoto nchini Italia wamesema kuwa tukio hilo limetokea alfajiri ya Jumamosi Disemba nane mwaka huu katika klabu ya Lanterna Azzurra iliyopo kwenye mji wa Corinaldo.
Habari zaidi kutoka nchini Italia zinasema kuwa, watu hao waliokufa ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 na kwamba wengi wa waliojeruhiwa hali zao ni mbaya.
Sababu za watu hao kukanyagana katika klabu hiyo ya usiku ya Lanterna Azzurra bado hazijafahamika, lakini taarifa za awali zinasema kuwa walikuwa wakijaribu kukimbia baada ya mtu mmoja kupuliza gesi ya kutoa machozi.