Shamima kuvuliwa uraia wa Uingereza

0
680

Serikali ya Uingereza imemvua uraia wa nchi hiyo msichana Shamima Begum  aliyejiunga na Wanamgambo wa IS  wa nchini Syria akiwa na umri wa miaka Kumi na Mitano.

Habari kutoka nchini Uingereza zinasema kuwa Shamima ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 19, ana nafasi ya kupata uraia wa nchi nyingine hata kama ameukosa Uraia wa nchi hiyo.

Hata hivyo familia ya  Shamima  kupitia kwa Wakili wake imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo na inatathmini njia sahihi za kisheria za kufuatia ili kupinga uamuzi huo.

Uingereza imefikia uamuzi huo baada ya Shamima, aliyeondoka nchini humo mwaka 2015 kudai kuwa anataka kurejea nyumbani.

Shamima alipatikana katika kambi moja ya wakimbizi nchini Syria hivi karibuni  baada ya kuondoka katika mji wa Baghuz, mji ambao ni moja ya ngome za Wanamgambo wa IS na ameondoka kwa Wanamgambo hao akiwa na mtoto mchanga wa kiume aliyejifungua siku chache zilizopita.

Katika maelezo yake Shamima mwenye asili ya Bangladeshi amesema kuwa,  alisafiri kwenda nchini Syria akitumia hati ya kusafiria ya dada yake ya Uingereza, lakini alinyang’anywa alipovuka mpaka.

Aliondoka nchini Uingereza na rafiki zake wawili, Kadiza Sultana na Amira Abase  na inadhaniwa huenda Sultana alikufa baada ya nyumba moja alimokua akiishi nchini Syria kulipuliwa,  na Abase hajulikani alipo hadi sasa.