Wakazi wa Jimbo la Victoria, Australia wametakiwa kuondoka kwenye makazi yao ili kuepuka kukumbwa na moto unaoendelea kuwaka, huku mamlaka ya hali ya hewa ikitangaza kuwa leo ijumaa kiwango cha joto kitaongezeka pamoja na upepo mkali.
Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison amesema hali hiyo inatarajiwa kuwa mbaya kwenye majimbo ya mashariki ya nchi hiyo na kubainisha kuwa meli mbili tayari zipo katika pwani ya jimbo la Wales lililoathiriwa vibaya kutoa msaada wa kuhamisha watu .
Wakati huo huo, maelfu ya wananchi wameandamana kutokana na nchi hiyo kushindwa kupatia ufumbuzi mabadiliko hayo ya tabianchi.
Morrison amesema nchi hiyo ipo njiani kumaliza tatizo hilo la moto ambapo vikosi vya zimamoto kutoka Marekani, Canada na New Zealand tayari vipo nchini humo kusaidia kuzima moto huo.
Jumla ya watu 27 wamefariki dunia huku makazi na mali mbalimbali zikiteketezwa au kuharibiwa na moto huo ulioanza mwishoni mwa Julai 2019.