Saudi Arabia yakiri kupangwa kwa mauaji ya Khashoggi

0
1985

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudi Arabia, – Saud Al-Mojeb amesema kuwa mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi yalipangwa.

Taarifa  ya Al-Mojeb inakinzana na ile iliyotolewa awali kwamba Khashoggi aliuawa kwa bahati mbaya akiwa kwenye ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Instanbul nchini Uturuki.

Katika taarifa hiyo ya awali, maafisa wa Saudi Arabia pia walidai kwamba Khashoggi aliingia na baadaye aliondoka katika ubalozi huo mdogo.

Kauli hiyo ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudi Arabia inaashiria kuwa watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi walifanya kitendo hicho kwa kudhamiria.

Habari zaidi kuhusu mauaji hayo ya Kashoggi zinasema kuwa Kansela wa Ujerumani, -Angela Merkel amezungumza na mwana mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed Salman na kulaani mauaji hayo.

Merkel ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa haraka, wa wazi na wenye kuaminika kuhusu tukio hilo na wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.