Samaki mkubwa zaidi

0
230

Samaki mwenye uzito wa kilo 300 aliyevuliwa katika mto Mekong nchini Cambodia, ametajwa kuwa ni samaki mkubwa zaidi wa maji baridi kuwahi kuvuliwa duniani.

Wanakijiji wanaoishi jirani na mto Mekong wamempa samaki huyo jina la Boramy likiwa na maana ya Mwezi Mzima katika lugha ya Khmer, na hiyo ni kutokana na umbo lake kuwa la duara.

Samaki huyo ambaye ametambuliwa na wanasayansi nchini Cambodia kuwa ni wa jinsia ya kike, ana urefu wa mita nne na alirudishwa mtoni mara baada ya kuwekewa alama za kielektroniki ili kuruhusu wanasayansi kufuatilia mienendo na tabia zake.

Samaki huyo aina ya Stingray amempita samaki aina ya Kambare mwenye uzito wa kilo 293 aliyevuliwa nchini Thailand mwaka wa 2005, ambaye alikuwa akishikilia rekodi ya kuwa samaki mkubwa duniani kuwahi kuvuliwa katika maji baridi.

“Katika miaka 20 ya kutafiti samaki wakubwa katika mito na maziwa kwenye mabara sita, huyu ndiye samaki mkubwa zaidi wa maji baridi ambaye tumekutana naye au ambaye amerekodiwa mahali popote ulimwenguni.” amesema Zeb Hogan mmoja wa watafiti

Samaki ‘Stingray’ ambaye ni mkubwa zaidi kuvuliwa katika maji baridi inaelezwa kuwa yupo hatarini kutoweka.

Samaki huyo ni wa pili kuchunguzwa na timu ya watafiti tangu mwezi Mei mwaka huu ambapo samaki wa awali kupatikana alikuwa na uzito wa kilo 181.

Je nini kifanyike ili kuboresha utafiti wa vyumbe wa baharini?.