Ruto: Sitalipiza kisasi kwa yaliyotokea nyuma

0
155

Rais Mteule wa Kenya, William Ruto amesema kwamba amewasamehe wote na wakati akielekea kuanza kuiongoza Kenya, hatokuwa na kisasi na kwamba atashirikiana na kila mtu katika kuijenga Kenya iliyo moja na imara zaidi.

Ruto ambaye ni Naibu Rais wa Kenya amesema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais, katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa huku utangazaji matokeo ukighubikwa na sintofahamu kubwa.

Katika salamu zake amewashukuru mamilioni ya Wakenya waliompigia kura na wale waliopigia wagombea wengine, akisema kwamba kwa matokeo hayo Kenya imeshinda.

Licha ya Rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga kwenye uchaguzi, Ruto amemshukuru Kenyatta kwa muda wote wa miaka 10 waliofanya kazi pamoja katika kuiongoza Kenya.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati amemtangaza Ruto kuwa mshindi baada ya kupata kura halali 7,176,141 sawa na asilimia 50.49%. Kwa matokeo hayo Ruto ametimiza takwa la kisheria la kupata walau asilimia 50+1 ya kura halali.

Chebukati amesema Raila Odinga amepata kura 6,942,930 (48.85%), George Wajackoyah 61,969 (0.44%) na Waihiga Mwaure – 31,987 (0.23%).